Ripoti Iliyowasilishwa Inasema Wanajeshi Wa Australia Walitenda Uhalifu Wa Kivita Afghanistan

 

Uchunguzi juu ya uhalifu wa kivita uliofanywa na wanajeshi wa Australia nchini Afghanistan umegunduwa kwamba kwa uchache raia na wafungwa 39 waliuawa kinyume na sheria, kwa mujibu wa mkuu wa majeshi wa Australia. 

Akiwasilisha muhtasari wa ripoti ya uchunguzi wa miaka minne mbele ya waandishi wa habari mjini Canberra siku ya Alkhamis (Novemba 19), Mkuu wa Jeshi la Australia Angus Campbell alisema kikosi maalum cha jeshi la Australia kilihusika na mauaji hayo dhidi ya wafungwa, wakulima na raia wa kawaida.

Jenerali Campbell alisema kuna rikodi za kutia aibu kama vile mwanajeshi kumuuwa mfungwa ili tu kupata ladha ya kumuuwa mtu wa kwanza, tendo ambalo kijeshi huitwa "kumwaga damu", na kisha baada ya mauaji kama hayo, wanajeshi walikuwa wakipandikiza silaha na redio ili kutunga madai ya uongo kwamba wahanga wao walikuwa maadui waliouawa kwenye mapambano.

Hata hivyio, kwenye mkutano huo na waandishi wa habari, mkuu huyo wa majeshi alisema kilichotendwa na wanajeshi hao wachache, hakiwakilishi maadili ya walio wengi kwenye jeshi la Australia.

"Alichogunduwa Inspekta Mkuu kinakinzana kabisa na juhudi nzuri na kinaathiri mamlaka yetu ya kimaadili kama jeshi. 

Ripoti yake inaeleza kwa udani taarifa zinazohusiana na tuhuma zinazoumiza sana za mauaji ya kinyume cha sheria yaliyofanywa na baadhi yetu. Kwa heshima zote nawaomba watu wa Australia kuwakumbuka na kuwaamini wengi waliosalia. Nami naamini hivyo."

Campbell alisema mauaji hayo haramu yalianza mwaka 2009, ingawa mengi yao yalifanyika mwaka 2012 na 2013. 


EmoticonEmoticon