Vyombo vya
habari vya kibinafsi nchini Uganda, vimekataa kupeperusha hotuba ya rais Yoweri
Museveni ambayo alikuwa amepanga kufanya kila Jumapili, kuanzia saa moja kamili
jioni hadi saa tatu usiku saa za Kampala.
Museveni alikuwa ameagiza
vyombo vyote vya habari nchini Uganda kupeperusha hotuba yake ya kila wiki,
lakini muungano wa wamiliki wa vyombo hivyo umekataa agizo hilo wakisema huu ni
msimu wa kampeni na kwamba hawawezi kutoa fursa kwa mgombea mmoja pekee bila
kuzingatia wagombea wengine kwa sababu inavunja kanuni za uandishi wa habari.
Taarifa ya muungano wa
wamiliki wa vyombi vya habari Uganda umeandikia tume ya mawasiliano Uganda –
UCC, ukisema kwamba “Museveni ni mgombea wa urais katika uchaguzi mkuu mwa
mwaka 2021 na kwa hivyo tukipeperusha hotuba yake, wasikilizaji na watazamaji
watachukulia ujumbe wake kama kampeni.” Ameandika katibu wa muungano huo Joseph
Beyanga.
Kulingana na sheria ya
utangazaji nchini Uganda ya mwaka 2013, kila mgombea katika uchaguzi anastahili
kupewa nafasi sawa katika vipindi na habari zinazochapishwa au kupeperushwa na
vyombo vyote vya habari nchini humo.
Kulingana na msemaji wa
Museveni, Don Wanyama, hotuba ya Museveni ya jumapili ilikuwa imepangiwa
kuangazia usalama na ukuaji wa uchumi.
Baada ya muungano wa
vyombo vya habari kukataa kupeperusha hotuba hiyo, Wanyama aliandika ujumbe wa
twitter kwamba “hotuba ya rais imeahirishwa hadi siku ambayo tutawaarifu.
Tunasikitika kwa usmbufu wowote ambao umejitokeza.”
“Tungependa kujua aina ya hotuba atakayotoa rais Museveni kabla ya kupanga namna ya kuipeperusha. Iwapo hotuba hiyo ni kampeni, basi vyombo vya habari vinavyotaka kuipeperushwa vinastahili kulipwa kwanza.” Imesema barua ya muungano wa wamiliki wa vyombo vya habari kwa mamalaka ya mawasiliano UCC. Maafisa wa UCC hawajajibu barua hiyo.
EmoticonEmoticon