Wafuasi Wa Trump Waandamana Wakidai Udanganyifu Wa Uchaguzi

 

Maelfu ya wafuasi wa Donald Trump wameandama Washington kumuunga mkono kiongozi huyo anayemaliza muda wake. Maafisa wa Marekani wametupilia mbali madai ya Trump ya kutokea udanganyifu katika uchaguzi wa Novemba 3. 

Maelfu ya wafuasi wa Rais Donald Trump wameandamana Jumamosi mjini Washington, Marekani, huku wakiimba nyimbo za kudai kiongozi huyo anafaa kuendelea kubakia madarakani kwa miaka mengine minne.

Trump na wafuasi wake wanadai kwamba kulifanyika udanganyifu kwenye uchaguzi wa Novemba 3, uliopelekea rais huyo kushindwa na Rais mteule Joe Biden, na kulazimika kuondoka Ikulu baada ya muhula mmoja tu madarakani.

Trump binafsi na msafara wake wa magari alipita katikakati ya maandamano hayo akiwa njiani akielekea kwenda kucheza gofu, huku wafuasi wake wakimshangilia naye akiwaonyesha tabasamu.

Watu wasiopungua 10,000, ambao wachache walikuwa wamevaa barakoa, walikutana katika ukumbi wa Freedom Plaza kabla ya kuandamana hadi katika mahakama kuu huku wakipeperusha bendera za kumuunga mkono Trump.

"Tulitaka kumuonyesha kuwa tunamuunga mkono, tunahisi wanajaribu kuiba uchaguzi," amesema Pam Ross, akimaanisha wapinzani wa kisiasa wa rais Trump, ambaye aliendesha gari kwa masaa nane kutoka Ohio kuja kushiriki maandamano hayo.

Kiongozi huyo wa Republican anashikilia madai yake kwamba kulifanyika udanganyifu na kwamba alimshinda Biden katika uchaguzi wa Novemba 3.


EmoticonEmoticon