Waziri Mkuu Wa Ethiopia Aagiza Jeshi Kuzima Maasi

 

Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed amesema ameamuru jeshi kutekeleza wajibu wake wa kuliokoa taifa na Umma katika jimbo la kaskazini la Tigray baada ya kukishutumu chama cha TPLF ambacho kimekuwa kikiongoza jimbo hilo tangu mwanzoni mwa miaka ya 90 kwa 'kuanzisha vita.'

Waziri Mkuu amekishutumu chama cha TPLF kwa kushambulia ngome ya kijeshi katika jimbo hilo. Hilo limekuja baada ya miezi kadhaa ya kuwepo kwa mvutano kati ya serikali kuu mjini Addis Ababa na mamlaka ya jimbo la Tigray.

TPLF awali ilishutumu utawala wa Abiy kwa kutumia janga la virusi vya corona kama sababu ya kusalia madarakani baada ya utawala wake kisheria kuisha mwanzoni mwa mwezi Oktoba. Serikali ya nchi hiyo mara kwa mara imekuwa ikikilaumu TPLF kusababisha vurugu nchi nzima.

Kwa mujimu wa taasisi inayoangalia uhuru wa mtandao , Netblocks kumekuwa na hali ya kuzimwa kwa data za mtandao na simu mapema asubuhi siku ya Jumatano jimboni Tigray. Taarifa ya Waziri Mkuu imesema kuwa ''mpaka umevukwa'' na kuwa kuiokoa nchi hiyo na Umma kwa ujumla, matumizi ya nguvu yamekuwa chaguo la mwisho,'' dhidi ya TPLF.


EmoticonEmoticon