Waziri mkuu
wa Ethiopia Abiy Ahmed, ametoa muda wa mwisho kwa majeshi ya jimbo la Tigray
kujisalimisha au wakabiliwe na hatua za kijeshi katika mji mkuu wa jimbo hilo
wa Mekele.
Katika taarifa yake
iliyowalenga viongozi wa chama cha TPLF, Abiy amewasihi wapiganaji hao
kujisalimisha kwa amani ndani ya saa 72, akisema kwamba safari yao imefika mwisho.
Ameendelea kusema kwamba
wapiganaji hao wapo katika hali ambayo hawawezi kutoroka na kuwataka wachukue
fursa hiyo ya mwisho.
Jeshi la Ethiopia limekuwa
likipigana na majeshi ya Tigray tangu vita mzozo ulipozuka Novemba 4 wakati
Abiy alipotuma wanajeshi wa kitaifa katika eneo hilo.
Serikali ya Ethiopia
inalishutumu jeshi la Tigray kwa kushambulia kambi ya jeshi la kitaifa katika
eneo la Tigray.
Mamia ya watu wameuawa na
maelfu kukimbilia Sudan tangu vita hivyo vilipoanza.
Mawasiliano yamekatwa
katika eneo hilo, huduma ya internet hamna kabisa na kufanya vigumu kwa
waandishi wa habari kupata uthibitisho wa idadi ya vifo na ripoti za ghasia.
Jimbo la Tigray lenye
maeneo tisa, liko kaskazini mwa Ethiopia.
Hali ya wasiwasi imekuwa ikiongezeka katika eneo hilo tangu Septemba 9 baada ya viongozi wa Tigray kuandaa uchaguzi licha ya Abiy Ahmed kuahirisha uchaguzi huo kutokana na janga la virusi vya Corona.
EmoticonEmoticon