Wimbi Jipya La COVID-19 Lazusha Taharuki Barani Ulaya

 

Hasira na wasiwasi unaongezeka miongoni mwa wakaazi wa mataifa mengi barani Ulaya kutokana na kurejea tena kwa vizuizi vikali vya kukabiliana na maambukizi pamoja na vifo vya COVID-19. 

Katika kile kinachoonekana kuwa ishara za kukata tamaa, waandamanaji kwenye miji kadhaa nchini Uhispania mwishoni mwa wiki walipambana na vikosi vya usalama kupinga kurejeshwa kwa marufuku ya shughuli za kawaida kujaribu kupambana na kitsho cha virusi vya corona.

Hivi sasa Uhispania inatekeleza amri ya kutotoka nje usiku na karibu majimbo yote ya nchi hiyo yameifunga mipaka ya ndani kuzuia safari za masafa marefu.

Serikali barani Ulaya zinahangaika kupunguza ongezeko la kutisha la maambukizi ya virusi vya corona ambayo hadi sasa yamesababisha vifo vya watu 279,000 barani humo tangu vilipozuka nchini China mwishoni mwa mwaka 2019.

Nchini Uingereza, wengi wameelezea wasiwasi walio nao kuhusu hasara ya kiuchumi itakayopatikana katika muda wa wiki nne ambao shughuli zote za kawaida zitafungwa.

Huko Italia ambako kulishuhudiwa maandamano makubwa wiki iliyopita, serikali inatarajiwa kutengaza hatua mpya za vizuizi baadae hivi leo.

Duru zimearifu serikali inalenga kupiga marufuku safari baina ya majimbo nchini humo, kufunga maduka makubwa, kupunguza shughuli za biashara na kuzuia watu kutoka nje usiku.


EmoticonEmoticon