Yoweri Museveni Kusimamia Mazungumzo Ya Kuleta Amani Ethiopia

 

Rais wa Uganda Yoweri Museveni atasimamia mazungumzo ya kuleta amani nchini Ethiopia kati ya serikali na maafisa wa eneo la Tigray.

Kulingana shirika la habari la AFP, maafisa wa serikali ya Ethiopia wasiotaka kutajwa wamesema kwamba mazungumzo hayo yamepangwa kuanza Jumatatu, kaskazini mwa Uganda.

Naibu waziri mkuu wa Ethiopia Demeke Mekonnen Hassen, ambaye pia ni waziri wa mambo ya nje, pamoja na wawakilishi wa Tigray, wanatarajiwa nchini Uganda Jumatatu kwa mazungumzo hayo.

Hayo yanajiri wakati kiongozi wa eneo lililojitenga nchini Ethiopia, Tigray, amethibitisha kwamba wapiganaji wake walifanya mashambulizi ya roketi kwenye uwanja wa ndege katika mji mkuu wa Eritrea.

Shambulizi hilo linaongeza wasiwasi wa kusambaa kwa vita katika eneo hilo la pembe ya Afrika.

Debretsion Gebremichael, amesema kwamba wapiganaji wake walishambuliwa kila upande na maelfu ya wanajeshi wa Eritrea na vifaru anavyodai waliingia Tigray kuwasaidia wanajeshi wa Ethiopia.

Wanadiplomasia waliwaambia waandishi wa habari Jumamosi usiku kuwa makombora mengi yalipiga Asmara, yakitua karibu na uwanja wa ndege, ingawa vizuizi vya mawasiliano huko Tigray na Eritrea vilifanya ripoti hizo vigumu kuthibitisha.


EmoticonEmoticon