Afrika Kusini Yarejesha Hatua Za Kuzuia Kuenea Kwa COVID-19

 

Afrika Kusini imerejesha hatua kali za kuzuia maambukizi ya virusi vya corona kwa kupiga marufuku mikusanyiko, marufuku ya kutotoka nje usiku na uuzaji wa pombe wakati maambukizi yakipindukia milioni moja. 

Afrika Kusini imekuwa nchi ya kwanza barani Afrika ambapo visa vya maambukizi ya corona vimepindukia milioni moja. Wizara ya Afya ilitangaza kwamba iko katikati ya wimbi la pili la maambukizi, na zaidi ya visa milioni moja vya covid-19 vimesajiliwa tangu mwezi Machi.

Katika hotuba yake kwa taifa aliyoitoa kwa njia ya televisheni Jumatatu rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa ametangaza kurejeshwa kwa hatua za kukabiliana na maambukizi zilizoanza mara moja. 

Hatua hizo ni pamoja na marufuku ya kutotoka nje usiku, marufuku ya uuzaji pombe, kufungwa kwa migahawa yote na zuio la mikusanyiko ya watu.

"Kuanzia sasa, ni lazima kwa kila mtu kuvaa barakoa akiwa maeneo ya umma. Mtu atakayeshindwa kufunika mdomo na pua atakuwa anatenda kosa."

Kama ilivyo kwa Uingereza Afrika Kusini inapambana na aina mpya ya kirusi cha coronaambacho wataalamu wanadai kwamba kinasambaa zaidi kuliko cha hivi sasa. 

Chama cha wafanyakazi wa afya cha Afrika Kusini kinachowakilisha wauguzi na madaktari, kimeonya kwamba mfumo wa afya wa taifa hilo uko karibu kuzidiwa na mchanganyiko wa idadi kubwa ya wagonjwa wa covid-19 na wagonjwa wengine wanaohitaji huduma ya dharura.


EmoticonEmoticon