Bei Ya Chakula Ulimwenguni Imepanda Katikati Ya Janga La COVID

Bei ya chakula ulimwenguni imepanda kwa mwezi wa sita mfululizo, ikigonga kiwango cha juu kabisa tangu Desemba 2014, kulingana na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa FAO. 

Kulingana na shirika hilo la chakula la Umoja wa Mataifa, bei ya chakula imeongezeka mwezi Novemba kwa kiwango ambacho hakikuwahi kushuhudiwa kwa miaka sita.

Faharisi inayochapishwa kila mwezi na shirika hilo la FAO, hapo Alhamisi imedhihirisha kwamba bei za bidhaa kadhaa za chakula zimeongezeka mno mwezi Novemba.

Bidhaa ambayo imeongezeka bei zaidi ni mafuta ya kupikia. Kutokana na kupanda kwa bei ya mafuta ya mawese, bei ya mafuta ya kupikia imeongezeka kwa asilimia 14.5.

Bei za vyakula vya nafaka, sukari, nyama, na maziwa pia zimeongezeka.

Kiwango cha bei ya sukari kiliongezeka kwa asilimia 3.3% kutokana na kupungua kwa uzalishaji ulimwenguni kote. Hali mbaya ya hewa imedhofisha mavuno katika mataifa ya Umoja wa Ulaya, Urusi na Thailand.

Bei za mazao makuu ya nafaka zilipanda kwa wastani wa asilimia 2.5, ingawa bei zilikuwa zimepanda kwa asilimia 20 mwaka jana. Bei za nyama na maziwa hazukuongezeka sana.


EmoticonEmoticon