EU Yasema Hatua Zimepigwa Kuhusu Brexit Lakini Muafaka Bado

 

Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen amesema leo kuwa hawezi kusema kama muafaka utapatikana kati ya Umoja wa Ulaya na Uingereza lakini kumepigwa hatua katika mazungumzo yao na kwamba siku chache zijazo zitakuwa muhimu. 

Akilihutubia bunge la Ulaya mjini Brussels, von der Leyen amesema kufikia sasa wamepata suluhisho la masuala mengi yakiwemo ya uongozi, lakini bado kuna mambo mawili yanayohitaji ufumbuzi, ambayo ni kuweko mazingira sawa ya ushindani na suala la uvuvi. 

Uingereza inasisitiza kuwa na udhibiti wa mipaka yake ya bahari wakati Umoja wa Ulaya unataka kuruhusiwa kuitumia kwa ajili ya uvuvi. 

Uingereza ilijiondoa Umoja wa Ulaya Januari mwaka huu lakini pande hizo mbili zinajaribu kufikia makubaliano ambayo yatasimamia karibu dola trilioni moja za biashara kwa mwaka, kabla ya uwanachama usio rasmi - unaofahamika kama kipindi cha mpito - kumalizika Desemba 31.


EmoticonEmoticon