Kampuni ya
Marekani ya Google, imeiambia serikali ya Uganda kuwasilisha kesi mahakamani
kuhusiana na ombi lake la kutaka kufunga stesheni kadhaa za televisheni
zinazopeperusha matangazo yake kupitia You tube.
Serikali ya
Uganda kupitia mamlaka ya mawasiliano nchini humo UCC, iliandikia Google
ikitaka kampuni hiyo kufunga stesheni ya Ghetto TV na nyingine 13 kwa madai
kwamba zimekiuka maadili na kuvunja sheria za upeperushaji habari nchini humo.
Ghetto TV na
stesheni nyingine kadhaa, zina uhusiano na chama cha National Unity Platform,
chake mgombea wa urais Robert Kyagulanyi maarufu Bobi Wine.
Kulingana na
vyombo vya habari nchini Uganda, kiongozi wa mawasiliano wa kampuni ya Google
barani Afrika Dorothy Ooko, amesema kwamba kampuni hiyo haiwezi kufunga
stesheni hizo kwa sababu tu kwamba serikali imetaka ifanyike hivyo.
“Ni vigumu
sana kuondoa tu stesheni kwa sababu serikali nataka stesheni hiyo iondolewe
kwenye You tube. Tunafuata sheria kila mara, lakini ni lazima iwe amri kutoka
mahakamani. Barua zinaonyesha tu yake UCC imewasilisha kwa ubalozi. Sio amri ya
mahakama,” amesema Oooko.
Ombi la
serikali linajiri wakati kampeni kuelekea uchaguzi mkuu wa Januari 14
zinaendelea. Mgombea wa urais Robert Kyagulanyi amepata wafuasi wengi sana
kupitia mitandao ya kijamii kama Facebook na You tube.
Barua ya UCC
kwa Google inasema kwamba “tume ya mawasiliano ya Uganda imepokea malalamiko
kadhaa kutoka kwa maafisa wa serikali akiwemo waziri wa mambo ya ndani,
mwenyekiti wa usalama wa taifa, polisi na jeshi la nchi hiyo kuhusu habari
zinazopeperushwa na vituo hivyo vinavyotumia You tube na kwamba vinapeperusha
habari ambazo zinavunja sheria ya mawasiliano ya Uganda, ya mwaka 2013 na
sheria inayosimamia habari ya mwaka 2019, ibara ya 8 sehemu ya 2.”
Televisheni
ambazo zimetajwa kwenye barua ya UCC ni pamoja na TMO Online, Lumbuye Fred,
Trending Channel Ug, Uganda Yaffe, Uganda News Updates, Ghetto TV, Busesa Media
Updates, Uganda Empya, Map Mediya TV, KK TV, Ekyooto TV, Namungo Media, JB
Muwonge na Bobi Wine 2021.
Barua hiyo inadai kwamba televisheni hizo kwenye mtandao wa You tube, zilitumika kueneza machafuko ya hivi karibuni nchini Uganda yaliyopelekea vifo vya watu kadhaa na uharibifu wa mali.
EmoticonEmoticon