Joe Biden Aahidi Chanjo Milioni 100 Za COVID-19

 

Rais mteule wa Marekani Joe Biden ameuainisha mpango wake wa kupambana na janga la virusi vya corona katika siku zake 100 za mwanzo za urais huku akiahidi kwamba serikali yake itatoa chanjo milioni 100 kote nchini humo. 

Kwenye kikao kilichofanyika Wilmington, Delaware, Biden amesema ataliomba bunge kuruhusu ufadhili kamili wa mchakato wa kusambaza chanjo kote nchini humo na kuongeza kuwa katika siku zake 100 za mwanzo za urais wake, kwa pamoja wataweza kubadilisha mkondo wa ugonjwa huo nchini humo, lakini pia hali ya Waamerika.

Biden ambaye pia aliitambulisha timu yake ya afya ya umma, amesema kuwarejesha watoto shuleni, ni suala ambalo serikali yake italipatia kipaumbele.

"Jambo la tatu ambalo nitaomba katika siku 100, litakuwa ni kipaumbele cha kitaifa cha kuwarudisha watoto wetu shuleni. Na ikiwa bunge litatoa ufadhili tunahitaji kuwalinda wanafunzi, waalimu na wafanyakazi... ikiwa majimbo na miji pia itaweka hatua madhubuti za afya ya umma na sisi sote tukazifuata, basi timu yangu itahakikisha kuona kwamba shule zetu nyingi zinaweza kuwa zimefunguliwa hadi mwishoni mwa siku zangu 100 za kwanza." alisema Biden.


EmoticonEmoticon