Joe Biden Awataka Wamarekani Kuvaa Barakoa Kwa Siku 100

 

Rais mteule wa Marekani amesema atawaomba raia wa Marekani kuvaa barakoa siku 100 za mwanzo za utawala wake ili kupunguza maambukizi ya virusi vya corona. Katika mahojiano aliyoyafanya na Jake Tapper wa CNN, bwana Biden alisema: "Siku ya kwanza nitakayoapishwa nitawaomba wananchi kuvaa barakoa kwa siku 100 na sio milele.

"Na nadhani itaweza kusaidi kupunguza maambukizi kwa kiasi kikubwa sana, kama chanjo na barakoa zitaweza kupunguza maambukizi." 

Wataalam wa katiba wanasema rais wa Marekani hana mamlaka ya kutoa amri kwa watu kuvaa barakoa lakini bwana Biden alisema wakati wa mahojiano hayo kuwa makamu wake wa rais Kamala Harris ataweka mfano wa namna ya kufunika uso.

Mamlaka ya rais yanahusisha kulinda mali za serikali ya Marekani, na bwana Biden aliiambia CNN kuwa ana lengo la kutumia mamlaka hayo.

"Ninaenda kutoa agizo katika serikali ya shirikisho kuwa wanapashwa kuvaa barakoa," alisema.

Aliongeza: "Katika upande wa usafirishaji,kila mtu anapaswa kuvaa barakoa kwenye ndege na mabasi na usafiri wowote."

Ndege za Marekani , uwanja wa ndege na maeneo mengi ya umma tayari yanawataka abiria na wafanyakazi wake kuvaa barakoa. White House ya Trump imekataa kufuata agizo hilo kutoka kwa wataalamu wa afya.

Alizungumza huku Gavana wa California Gavin Newsom akitoa amri ya kukaa nyumbani kwa sehemu kubwa ya wakazi wa jimbo lake , akisema ana weka ''mapumziko ya dharura " huku wagonjwa wa virusi wakitishia kupita uwezo wa hospitali .


EmoticonEmoticon