Kansela Wa Ujerumani Akiri Mwaka 2020 Kuwa Mgumu Katika Uongozi Wake

 

Kansela Angela Merkel katika hotuba yake mwaka mpya kwa Ujerumani, amewashambulia wale wanaopinga uwepo wa virusi vya corona, amesisitiza umuhimu wa umoja miongoni mwa jamii tofauti na pia ametoa ujumbe wa matumaini. 

Kansela huyo wa Ujerumani amesema bayana kwamba mwaka mzima wa 2020 ndio umekuwa mwaka wenye changamoto chungunzima katika uongozi wake wa miaka 15.

"Sidhani kama natia chumvi ninaposema: hakuna mwaka ambao umekuwa mgumu katika miaka yangu 15 ya uongozi kama mwaka huu unaoelekea kuisha," alisema Merkel katika hotuba hiyo ya kila mwaka inayosikilizwa na kutazamwa na mamilioni ya watu.

Katika janga ambalo limeukumba ulimwengu mzima, Wajerumani milioni 1.7 wameambukizwa virusi vya corona na wengine 32,000 kufariki dunia. 

Na idadi inaongezeka kwani mnamo Jumatano zaidi ya watu elfu moja walifariki katika kipindi cha saa ishirini na nne hiyo ikiwa ni mara ya kwanza tangu kuanza kwa janga lenyewe.

"Janga la virusi vya corona ndio changamoto kubwa ya kisiasa, kijamii na kiuchumi ya karne hii," amekiri Merkel. "Ni mzozo wa kihistoria ambao umehitaji mengi kutoka kwetu sote na mengi zaidi kwa baadhi ya watu, najua suala hili linahitaji uaminifu na subra kubwa kutoka kwenu, kutahitajika mwonyesho wa nguvu zaidi na kwa hilo ninawashukuru kwa moyo wangu wote."


EmoticonEmoticon