Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Aonya Kuhusu Ongezeko La Joto Duniani

 

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres ameikosoa jamii kwa kushindwa kupambana na ongezeko la joto duniani na amesema uongozi wa Marekani ni muhimu katika kushughulikia dharura ya mabadiliko ya tabianchi. 

Katika hotuba yake aliyoitoa kwenye Chuo Kikuu cha Colombia, mjini New York, Marekani, Guterres ameonya kuwa hali ya sayari imevunjika na ubinadamu unasababisha vita vya asili.

Amesema viwango vya joto kali, ukame pamoja na bahari kufikia rekodi za juu za joto zinasababishwa na utunzaji mbaya wa mazingira unaofanywa na mwanadamu, na ametoa wito wa kutokuweko kwa gesi chafu ya kaboni. 

Amesema mapambano ya janga la mabadiliko ya tabianchi ni kipaumbele cha juu katika karne ya 21.

''Tunalazimika kuchukua haraka hatua tatu muhimu katika kuushughulikia mzozo wa hali ya hewa. Kwanza, tunahitaji kutokuwa na gesi chafu ya kaboni ndani ya miongo mitatu ijayo. 

Pili, tunapaswa kuweka sawa fedha za kimataifa nyuma ya Mkataba wa Paris, mwongozo wa ulimwengu wa hatua za kuchukua kupambana na mabadiliko ya tabianchi. 

Na tatu, lazima tufanikiwe kuilinda dunia na hasa watu na nchi zilizoko katika hatari zaidi kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi,'' alisisitiza Guterres.

Akizungumzia kitisho kikubwa cha mabadiliko ya tabianchi, mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amefafanua kuwa hakuna njia ya kulishughulikia suala la mabadiliko ya tabianchi bila uongozi wa Marekani.


EmoticonEmoticon