Marekani Kuanza Kutoa Chanjo Ya COVID-19 Jumatatu

Maafisa wa Marekani wamesema chanjo ya virusi vya corona iliyotengenezwa na kampuni mbili za Pfizer na BioNTech itaanza kutolewa kwa mara ya kwanza kesho Jumatatu siku kadhaa tangu matumizi yake yalipoidhinishwa. 

Jenerali wa Jeshi la Marekani anayesimamia usambazaji wa  chanjo hiyo, Gus Perna, amesema dozi za kwanza zitasafirishwa leo Jumapili na hapo kesho zoezi ya utoaji chanjo litaanza kwa asilimia 100.

Perna amearifu kuwa ifikapo kesho vituo vya kutolea chanjo 145 vitakuwa vimepokea shehena ya kwanza, huku vituo 425 vitapelekewa chanjo siku ya Jumanne na chanjo hiyo itapokelewa pia kwenye vituo vingine 66 siku ya Jumatano.

Kampuni inayotengeneza chanjo hiyo imesema inafanya kazi na washirika wengine kuanza kusafirisha chanjo kwa kutumia magari ya mizigo kutoka kwenye maghala yake yaliyoko kwenye majimbo Michigan na Wisconsin  kwenda majimbo yote 50 ya Marekani.

Chanjo hiyo ni lazima ihafidhiwe kwenye baridi ya nyuzi -70 C, hali inayoleta changamoto itakayotatuliwa kwa kutumia barafu na kontena maalum zilizotengenezwa kwa ajili ya kuhifadhi shehena yake.


EmoticonEmoticon