Mlinzi Wa Bobi Wine Auawa Katika Mazingira Tatanishi

 

Mlinzi wa mgombea wa urais Robert Kyagulanyi, maarufu Bobi Wine, amefariki duniani katika mazingira tatanishi Jumapili.

Ripoti za vyombo vya habari Uganda vinakariri mashahidi wakisema kwamba Francis Kalibala, aligongwa na gari la jeshi la Uganda UPDF wakati msafara wa Bobi Wine ulikuwa unarudi Kampala kutoka Masaka katika kampeni.

Katika taarifa kupitia mitandao ya kijamii Bobi Wine amesema “nasikitika kutangaza kifo cha mmoja wa walinzi wangu Francis Kalibala aliyegongwa na gari la jeshi namba H4DF 2382 ambalo liliziba njia karibu na Busega na kutuzuia kupita.” Ameandika Bobi Wine na kuongeza kusema“Francis amefariki mda mfupi baada ya kufika katika hospitali ya Rubaga.”

Lakini msemaji wa jeshi la Uganda Brig. Flavia Byekwaso amesema katika taarifa kwa vyombo vya habari kwamba Francis alianguka kutoka kwa gari lililokuwa linaendeshwa kwa mwendo wa kasi.

“Francis hakugongwa na gari la jeshi la UPDF. Alianguka kutoka kwa gari namba UBF 850Z .” amesema Byekwaso katika ujumbe wa twitter.

Credit : Voa


EmoticonEmoticon