Mwanasheria Mkuu Wa Marekani Asema Hakuna Ushahidi Wa Madai Ya Wizi Wa Kura Marekani

 

Mwanasheria Mkuu wa Marekani, William Barr amesema wizara ya sheria imechunguza madai ya udanganyifu katika uchaguzi wa Novemba 3 na haijapata ushahidi wowote kuthibitisha madai hayo yaliyotolewa na Rais Donald Trump. 

Akiyazungumzia madai yanayotolewa na timu ya kampeni na kisheria ya Rais Trump, Barr amesema hadi sasa hawajapata ushahidi wowote kuhusu udanganyifu katika kiwango ambacho kinaweza kuyaathiri matokeo yaliyompa ushindi Joe Biden. 

Matamshi hayo yanaonekana kama pigo kubwa kwa Trump, ambaye hajakubali kushindwa.

Barr amesema kwamba kumekuwa na madai kuhusu udanganyifu wa kimfumo na kwamba mashine zilipangwa mahsusi kwa ajili ya kuchakachua matokeo ya urais. 

Amesema wizara ya mambo ya ndani na wizara ya sheria zimeyachunguza madai hayo, lakini hazijapata ushahidi wowote unaoweza kuyathibitisha.

Kwa muda mrefu Barr amekuwa akionekana kuwa mtiifu kwa Rais Trump tangu alipochukua nafasi ya Jeff Sessions mwaka 2018, lakini kabla ya uchaguzi vyombo vya habari viliripoti kuhusu Trump kutoridhishwa na mwenendo wake kwamba hakuonesha juhudi katika harakati za kiongozi huyo kuchaguliwa tena kuiongoza Marekani.


EmoticonEmoticon