Putin Asema Urusi Ingetaka Kumuuwa Navalny Angekuwa Marehemu

 

Rais wa Urusi Vladimir Putin amesema ripoti za uchunguzi katika vyombo vya habari, ambazo ziliwahusisha maafisa wa usalama wa Urusi na jaribio la kumuuwa kwa sumu mpinzani mashuhuri wa kiongozi huyo, Alexei Navalny, zilikuwa mbinu ya kuwashambulia viongozi wa Urusi. 

Putin amesema kama serikali ingedhamiria kumuuwa mwanasiasa huyo wa upinzani hivi sasa angekuwa marehemu. 

Navalny aliugua ghafla akisafiri kwa ndege tarehe 20 Agosti mwaka huu, na alisafirishwa siku mbili baadaye akiwa katika hali ya nusu kaputi hadi Ujerumani alikopatiwa matibabu. 

Baada ya kuchukuliwa vipimo, shirika la kudhibiti silaha za kemikali lilitangazwa kuwa aliwekewa sumu aina ya Novichok iliyotengenezwa enzi za Umoja wa Kisovieti. 

Mwanzoni mwa wiki hii, makundi mawili ya uchunguzi ya Bellingcat na The Insider, yalichapisha ripoti ambamo yalidai kuwa makachero wa shirika la upelelezi la Urusi, FSB, wamekuwa wakimfuata Navalny katika safari zake tangu mwaka 2017.


EmoticonEmoticon