Shrika la Afya Duniani WHO limetahadharisha dhidi ya wasiwasi wa kupindukia kuhusu aina mpya ya virusi vya corona vinavyosamba kwa kasi kubwa, baada ya kugunduliwa nchini Uingereza na baadae Afrika Kusini.
Shirika hilo la WHO limesema ni kawaida ya virusi kufanya hivyo wakati wa janga, baada ya aina hiyo ya virusi kuzua taharuki kote ulimwenguni, hali iliyopelekea mataifa kadhaa kuweka vizuizi vya usafiri kwa Uingereza na Afrika Kusini.
Maafisa wa WHO wamesema hawana ushahidi wowote unaoonyesha
kwamba aina hiyo mpya ya virusi inawafanya watu kuwa wagonjwa zaidi au kuwa ni
mbaya zaidi kuliko virusi vilivyokuwepo awali vya ugonjwa wa COVID-19.
Ingawa WHO imethibitisha kwamba aina hiyo mpya inaonekana kuenea kwa kasi
zaidi.
"Kufikia
sasa, ingawa tumeona mabadiliko kadhaa katika virusi vya corona, hakuna hata
aina moja iliyoleta athari yoyote katika tiba zinazotumiwa kwa sasa, dawa au
chanjo inayoendelea kufanyiwa uchunguzi na matumaini yetu ni kwamba hali hii
itaendelea kuwa hivyo," amesema Mwanasayansi Mkuu wa WHO, Soumya
Swaminathan katika mkutano wa njia ya video huko Geneva.
Kulingana na WHO, chanjo zilizotengenezwa kupambana na COVID-19 zina uwezo wa kutoa kinga dhidi ya aina hiyo mpya ya virusi vya corona. Lakini uchunguzi zaidi unaendelea kufanywa na wanasayansi.
EmoticonEmoticon