Tume
inayosimamia mawasiliano nchini Uganda (UCC) imeandika barua kwa kampuni ya
Marekani ya Google, ikiitaka kampuni hiyo ifunge stesheni kadhaa za televisheni
zinazopeperusha matangazo yake kupitia You tube.
Miongoni mwa
stesheni hizo ni Ghetto TV, inayomilikiwa na chama cha National Unity Platform
(NUP), cha mgombea wa urais Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine.
UCC inataka
karibu stesheni 13 zinazopeperusha matangazo yake moja kwa moja kupitia You
tube, kufungwa kwa msingi kwamba zimekiuka sheria na maadili ya habari nchini
Uganda.
Barua ya UCC
kwa Google inasema kwamba “tume ya mawasiliano ya Uganda imepokea malalamiko
kadhaa kutoka kwa maafisa wa serikali akiwemo waziri wa mambo ya ndani,
mwenyekiti wa usalama wa taifa, polisi na jeshi la nchi hiyo kuhusu habari
zinazopeperushwa na vituo hivyo vinavyotumia You tube na kwamba vinapeperusha
habari ambazo zinavunja sheria ya mawasiliano ya Uganda, ya mwaka 2013 na
sheria inayosimamia habari ya mwaka 2019, ibara ya 8 sehemu ya 2.”
Televisheni
ambazo zimetajwa kwenye barua ya UCC ni pamoja na TMO Online, Lumbuye Fred,
Trending Channel Ug, Uganda Yaffe, Uganda News Updates, Ghetto TV, Busesa Media
Updates, Uganda Empya, Map Mediya TV, KK TV, Ekyooto TV, Namungo Media, JB
Muwonge na Bobi Wine 2021.
Barua hiyo
inadai kwamba televisheni hizo kwenye mtandao wa You tube, zilitumika kueneza
machafuko ya hivi karibuni nchini Uganda yaliyopelekea vifo vya watu kadhaa na
uharibifu wa mali.
Inaendelea
kusema kwamba zinatumika “kueneza habari za uongo, na maoni potofu kwa nia ya
kupotosha jamii, zikiwa na lengo la kusababisha ghasia kwa misingi ya kikabila
na kisiasa.”
Barua hiyo
inaongezea kwamba habari na maoni yanayopeperushwa na stesheni hizo “yana
upendeleo, yanaonyesha miili ya watu waliokufa, waliojeruhiwa vibaya, ajali
mbaya na zinaweza kusababisha wasiwasi mkubwa katika jamii.”
UCC inasema
kwamba televisheni hizo za mtandao wa You tube, hazina leseni ya kupeperusha
habari nchini Uganda.
Kulingana na
ibara ya 27 ya sheria ya maudhui nchini Uganda, hakuna mtu anaruhusiwa
kupeperusha habari bila ya kuwa na leseni ya tume ya mawasiliano ya nchi hiyo
na anayefanya hivyo anaweza kuhukumiwa mwaka mmoja gerezani, kulipa faini au
kulipa faini na kifungo cha mwaka mmoja gerezani.
“Kwa hivyo, kwa kuzingatia sheria ya mawasiliano ya mwaka 2013 namba 5(1) (b), (j), (x), 6 na 45, Tume inataka Google kufunga kabisa stesheni hizo,” inasema barua ya UCC kwa kampuni ya Google.
EmoticonEmoticon