Ufaransa Yathibitisha Mtu Wa Kwanza Mwenye Aina Mpya Ya Kirusi Cha Corona

 

Ufaransa imethibitisha kupata mtu wa kwanza mwenye maambukizo ya aina mpya ya kirusi cha corona ambacho kilizuka hivi karibuni nchini Uingereza. 

Kama ilivyokuwa kwa Ujerumani iliyogunduwa kirusi hicho juzi, mtu aliyepatikana na maambukizo hayo ni raia wa Ufaransa anayeishi Uingereza na ambaye aliwasili Paris akitokea London tarehe 19 Disemba. 

Hata hivyo, licha ya kugunduliwa na aina hiyo mpya ya kirusi, wizara ya afya ya Ufaransa imesema mapema leo kwamba mtu huyo haoneshi ishara yoyote ya maradhi. 

Aina hiyo mpya ya kirusi ambayo wataalamu wanahofia kwamba inasambaa kwa kasi zaidi, imesababaisha zaidi ya mataifa 50 duniani kupiga marufuku ya safari kwa Uingereza. 

Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson amesema aina hiyo mpya ya kirusi cha corona ina asimilia 70 zaidi za kuambukiza na kusambaa kuliko kirusi cha awali. 

Uingereza imeshapoteza zaidi ya watu 68,000 hadi sasa kutokana na maradhi ya COVID-19 na kuifanya kuwa miongoni mwa mataifa ya Ulaya yaliyoathirika zaidi na janga hilo la kilimwengu.


EmoticonEmoticon