Ulimwengu Waadhimisha Miaka Mitano Ya Mkataba Wa Paris

 

Viongozi wa dunia wanatarajiwa kutangaza malengo mapana zaidi ya kudhibiti ongezeko la joto duniani katika maadhimisho ya miaka mitano ya mkataba wa kihistoria wa kupambana na mabadiliko ya tabianchi wa mjini Paris. 

Mkutano wa kilele utakaofanyika leo kwa njia ya mtandao unakuja wakati Umoja wa Mataifa umetahadharisha kuwa ahadi za sasa zilizotolewa na mataifa duniani kuzuia kupanda kwa kiwango cha joto bado hazitoshi.

Uingereza, Ufaransa na Umoja wa Mataifa ndiyo wenyeji wa mkutano huo ambao utafunguliwa rasmi na waziri mkuu wa Uingereza Boris Johnson baadae leo mchana.

Rais wa China Xi Jinpinga na wa Ufaransa Emmanuel Macron ni miongoni mwa viongozi wakuu wa mataifa wanaoshiriki, huku nafasi ya kuzungumza imetolewa kwa viongozi wa mataifa yaliyowasilisha ahadi pana zaidi za kuzuia utoaji wa gesi ya ukaa.

Mataifa hayo yanajumuisha Honduras na Guatemala, ambayo kwa pamoja hivi karibuni yalikumbwa na vimbunga pamoja na India inayokabaliwa na misimu ya mwaka isiyotabirika na uchafuzi mkubwa wa hewa.

Viongozi wa kampuni za biashara waliopangiwa kuzungumza ni pamoja na Tim Cook, afisa mtendaji mkuu wa kampuni ya Apple, ambayo imeahidi uzalishaji na usambazaji wa bidhaa zake utafikia lengo la matumizi ya nishati isiyochafua mazingira ifikapo mwaka 2030.


EmoticonEmoticon