Umoja Wa Mataifa Umesema Chakula Kimewaishia Wakaimbizi 100,000 Nchini Ethiopia

 

Umoja wa Mataifa umesema chakula sasa kimewaishia karibu wakimbizi 100,000 kutoka Eritrea ambao wamekuwa wakihifadhiwa katika kambi za jimbo la kaskazini mwa Ethiopia la Tigray, ambalo limezingirwa kwa karibu mwezi mzima kufuatia mapigano. 

Msemaji wa shirika la wakimbizi la Umoja wa Mataifa Babar Baloch amewaambia wanahabari jijini Geneva kuwa wasiwasi unaendelea kuongezeka kila saa kwa kuwa kambi hizo sasa hazina chakula na na hali hiyo inaiweka katika hatari kubwa ya kuzuka njaa na utapia mlo. 

Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed amefuta uwezekano wa mazungumzo na viongozi wa mkoa wa Tigray, ambao wamefurushwa lakini wanasema wanaendelea kupigana hata baada ya Abiy kutangaza ushindi katika mzozo huo. 

Umoja wa Mataifa unasema karibu watu milioni 2 mkoani Tigray sasa wanahitaji msaada na wengine milioni 1 wamekimbia makaazi, wakiwemo Waethiopia 45,000 walioingia nchini Sudan kama wakimbizi.


EmoticonEmoticon