Wakristo Waadhimisha Krismasi Huku Dunia Ikitatizwa Na Corona

 

Leo ni Sikukuu ya Krismasi, ambapo waumini wa dini ya Ukristo wanaadhimisha kuzaliwa kwa Yesu Kristo, lakini maadhimisho hayo mwaka huu yametandwa na janga la virusi vya corona linalozidi kuangamiza maisha ya watu. 

Hata kabla ya siku yenyewe kufika, tayari kiongozi mkuu wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis, alishatowa tamko la kuwataka waumini wa kanisa hilo kufuata maagizo yote ya mamlaka za kidunia juu ya kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona. 

Kiongozi wa kiroho wa Kanisa hilo kwenye Ukingo wa Magharibi, Pierbattista Pizzaballa, ametumia ibada ya Mkesha wa Krismasi kuiombea dunia iondokane na janga hilo. 

Kiongozi huyo alilazimika kuendesha misa ya Mkesha wa Krismasi mbele ya viongozi kidini pekee mjini Bethlehem, ambako inaaminika ndiko alikozaliwa Yesu Kristo. 

Hata Rais Mahmoud Abbas wa Palestina, ambaye kawaida huhudhuria maadhimisho hayo, safari hii ameshindwa kufika kwenye Kanisa la Nativity kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2005. 

Ukingo wa Magharibi umewekwa kwenye marufuku ya kutotoka nje kuanzia saa moja usiku hadi 12 asubuhi kwa wiki kadhaa sasa, ili kukabiliana na kasi ya maambukizo ya virusi vya corona. 

Eneo hilo linalokaliwa na Wapalestina milioni 4, limeshapoteza watu 800 hadi sasa kutokana na ugonjwa wa COVID-19.


EmoticonEmoticon