Walinda Amani Watatu Wa Burundi Wauawa Jamhuri Ya Afrika Ya Kati

 

Walinda amani watatu wa Umoja wa Mataifa wameuawa katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, huku nchi hiyo ikijiandaa kwa uchaguzi wa Jumapili (27 Disemba) na mapigano yakipamba moto kati ya vikosi vya serikali na waasi.

Taarifa iliyotolewa na Umoja wa Mataifa inasema kuwa wanajeshi hao wanatokea Burundi na kwamba wenzao wawili wamejeruhiwa kufuatia uvamizi dhidi ya vikosi vya Umoja wa Mataifa na vya serikali. 

Uvamizi huo ulifanyika kwenye mji wa Dekoa ulio katika mkoa wa Kemo na mji wa Bakouma kusini mwa mkoa wa Mbomou, ilisema taarifa hiyo bila kutaja undani zaidi.

Stephane Dujarric, msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, alilaani vikali mashambulizi hayo na kuzitaka mamlaka nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati kuchunguza kile alichokiita "uvamizi wa kikatili."

Pia alionya kwamba "mashambulizi dhidi ya walinda amani wa Umoja wa Mataifa yanaweza kuchukuliwa ni uhalifu wa kivita."

Taarifa hizo zimekuja katika wakati ambapo muungano wa waasi umetangaza kusitisha mapigano na kusema utaendelea na maandamano yake kwenye mji mkuu, Bangui, kufuatia kuwasili kwa vikosi vya Rwanda na Urusi kuilinda serikali ya taifa hilo lenye utajiri wa madini.


EmoticonEmoticon