Wataalam Wa Usalama Watia Shaka Madai Ya Utekaji Nyara Nigeria

 

Wataalam wa usalama wa Nigeria wanatia shaka madai ya maafisa kwamba uhasama kati ya wakulima na wafugaji wa ng'ombe ulisababisha wimbi la utekaji nyara hivi karibuni katika jimbo la Katsina lililopo kaskazini magharibi mwa nchi. Wanafunzi wavulana zaidi ya 300 walitekwa nyara mapema mwezi huu lakini baadaye wakaachiliwa huru.

Mamlaka huko Katsina mwanzoni ililaumu utekaji nyara wa wavulana wa shule 344 kwa magenge ya majambazi ambao wamewateka nyara baadhi ya watu kwa ajili ya kulipwa fidia katika jimbo la kaskazini magharibi mwa Nigeria.

Halafu maafisa walibadilisha usemi wao , wakidai utekaji huo unahusiana na mzozo kati ya wafugaji ng'ombe na wakulima juu ya matumizi ya ardhi.

Lakini kamishna mstaafu wa polisi na mchambuzi wa usalama Lawrence Alobi hakubaliani na wazo hilo kwamba wafugaji walifanya shambulizi hilo.

"Wafugaji hawana shida yoyote na wakuu wa shule au wanafunzi. Shida yao iko kwa wakulima, mahali ambako wanaweza kulisha ng'ombe wao. Kwa hivyo, sijui uhusiano kati ya utekaji nyara wa wanafunzi hao na mivutano na wakulima.” alisema Alobi.

Kikundi cha wanamgambo wa Kiislam Boko Haram kilidai kuhusika na utekaji nyara wa wavulana hao wa shule na kutoa picha ya video inayoonyesha baadhi ya wavulana waliotekwa kabla ya kuachiliwa huru.

Madai hayo, ikiwa yatathibitishwa, yangeashiria mabadiliko kwa kundi hilo, ambalo hadi sasa limekuwa likifanya kazi hasa katika upande wa kaskazini mashariki mwa nchi.


EmoticonEmoticon