Watu Zaidi Ya 37 Wapoteza Maisha Kwenye Ajali Ya Basi Cameroon

 

Zaidi ya watu 37 wamekufa leo na wengine 18 wamejeruhiwa vibaya baada ya basi la abiria walilokuwa wakisafiria kupata ajali katika kijiji cha Nemale magharibi mwa Cameroon. 

Basi hilo lenye uwezo wa kubeba watu 70 lilikuwa njiani kuelekea mji mkuu Yaounde kutoka mji wa magharibi wa Foumban wakati lilipogongana uso kwa uso na gari ya mizigo likijaribu kulikwepa kundi la watu. 

Afisa mwandamizi wa serikali ya eneo hilo Absalom Woloa amesema ajali hiyo imetokea usiku wa kuakia leo na wengi ya wasafiri walikuwa njiani kurudi nyumbani baada ya sikukuu ya Krismasi. Ameongeza kusema wakaazi wa kijiji katika eneo ajali ilipotokea waliwahi kutoa msaada kwa zaidi ya wasafiri 60 waliokuwemo ndani ya basi. 

Woloa pia amearifu kuwa idadi ya waliokufa inaweza kuongezeka katika wakati vikosi vya uokoaji vikiendelea kupekeua mabaki kwenye eneo la tukio.


EmoticonEmoticon