Biden Ajadili Mahusiano Imara Na Canada, Mexico Na Uingereza

 

Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson ameweka bayana kwa Rais Joe Biden Jumamosi kuwa ana nia ya kuanzisha makubaliano mapya ya kibiashara kati ya Marekani na Uingereza.

Hatua ya msukumo huo wa Johnson kufikia makubaliano imekuja wakati wa mazungumzo mapana kati ya viongozi hao yaliyo gusia ulimwengu kukabiliana na janga la virusi vya Corona na tangazo la uongozi wa Biden wiki hii kuwa Marekani itajiunga tena na mkataba wa Hali ya Hewa wa Paris na Shirika la Afya Duniani, kwa mujibu wa taarifa ya ofisi ya Johnson ya Downing Street.

Mkataba mpya wa kibiashara kati ya washirika ni kipaumbele cha juu kwa Johnson kuliko Biden. Uingereza imepata tena udhibiti wa sera yake ya taifa ya biashara mwanzoni mwa mwezi Januari baada ya kumalizika kipindi cha mpito cha Brexit.

Msemaji wa White House Jen Psaki alisema Ijumaa uongozi haukuwa na muda maalum wa kuanzisha makubaliano mapya ya kibiashara kwa sababu Biden yuko makini kwa kiasi kikubwa kuangazia kudhibiti janga la virusi vya corona na kushinikiza Bunge kupitisha mpango wa afueni wa athari za virusi vya corona wa dola trilioni 1.9.

Maongezi yake na Johnson ni takriban ya tatu ambayo Biden amefanya na viongozi wenzake tangu Ijumaa. Rais alizungumza pia na Waziri Mkuu wa Canada Justin Trudeau na Rais wa Mexico Andrés Manuel López Obrador Ijumaa jioni.


EmoticonEmoticon