Joe Biden Kusaini Maagizo Ya Kiutendaji Baada Ya Kuapishwa

 

Rais mteule wa Marekani, Joe Biden atasaini maagizo kadhaa ya kiutendaji siku ya kwanza baada ya kuapishwa kuiongoza nchi hiyo. 

Msaidizi wa ngazi ya juu wa Biden, Ron Klain amesema kwamba maagizo ya kiutendaji yatahusu janga la virusi vya corona, uchumi wa Marekani unaodorora, mabadiliko ya tabia nchi pamoja na ubaguzi wa rangi. ''Majanga yote haya yanahitaji kushughulikiwa haraka,'' alisema Klain ambaye ni mkuu wa watumishi ajaye wa Biden.

Kwa mujibu wa Klain, katika siku zake 10 za kwanza madarakani, Biden atachukua hatua madhubuti kushughulikia mizozo hiyo minne, kuzuia madhara mengine ya haraka na yasiyoweza kurekebishwa pamoja na kuirudisha nafasi ya Marekani ulimwenguni.

Marekani ina takriban watu 400,000 waliokufa kutokana na ugonjwa wa COVID-19 na nchi hiyo inarekodi zaidi ya visa vipya milioni moja kwa wiki, wakati ambapo virusi hivyo vinazidi kuenea. 

Wiki hii Biden aliuzindua mpango wa uokozi wa dola trilioni 1.9 kwa ajili ya kupambana na janga la virusi vya corona na kuufufua uchumi.

Klain amesema siku ya kuapishwa Biden, kama alivyoahidi atasaini maagizo ya rais ikiwemo ya Marekani kujiunga tena kwenye Mkataba wa Paris wa mabadiliko ya tabia nchi na kuibadili marufuku ya kuwazuia watu kutoka kwenye nchi kadhaa zenye waumini wengi wa Kiislamu kuingia Marekani, ambayo iliwekwa na Rais Donald Trump.


EmoticonEmoticon