Kiongozi Wa Iran Atishia Kumshambulia Trump

 

Kiongozi Mkuu wa kidini nchini Iran, Ayatollah Ali Khamenei, ameweka ujumbe mtandaoni akitoa wito Donald Trump ashambuliwe kama hatua ya kulipiza kisasi mauaji ya komanda wa juu wa jeshi, Jenerali wa kikosi maalum cha Iran Qasem Soleimani.

Picha kwenye tovuti yake rasmi inamuonesha aliyekuwa rais wa Marekani Donald Trump akicheza gofu katika kivuli cha ndege ya kivita au ndege kubwa isiyo na rubani.

Mtandao wa Twitter umefunga akaunti ambayo ilikuwa ya kwanza kuweka picha hiyo.

Msemaji wa mtandao huo amezungumza na shirika la Reuters na kusema akaunti hiyo - @khamenei_site - ilikuwa ni feki na ilikiuka kanuni za mtandao wa Twitter.

Hata hivyo, ujumbe huo ulitumwa tena na Ayatollah Khamenei katika akaunti ya Twitter kwa lugha ya Farsi yenye wafuasi zaidi ya 300,000. Na tangu wakati huo haionekani tena. 

Katika ujumbe huo wa Twitter ulioandikwa kwa lugha ya Farsi, neno "kulipiza kisasi" limewekwa kwa rangi nyekundu huku ujumbe mwingine ukisema: "Muuaji wa Soleimani na aliyeagiza kutekelezwa kwa mauaji hayo lazima watalipa".

Katika mtandao rasmi wa Ayatollah Khamenei, picha hiyo imewekwa na kuoneshwa kuwa muhimu. Na maneno yaliofuata ni matamshi yake aliyotoa Desemba 16, akiahidi tena kulipiza kisasi "muda wowote ule".

Mtandao wa Twitter uliombwa kuchukua hatua baada ya watumiaji kuchukulia hilo kama upendeleo wakidai kuwa Bwana Trump alifungiwa kutotumia mtandao huo, mbona isiwe vivyo hivyo kwa kiongozi huyo wa Iran.

Mtandao wa Twitter ulifunga akaunti ya Trump iliyokuwa na ushawishi mkubwa mapema mwezi huu baada ya yeye kuweka ujumbe ulioshawishi uvamizi na bunge la Marekani.

"Inawezekanaje huyu mnafiki anaweza kutoa wito wa mauaji ya aliyekuwa rais wa Marekani tena wazi kabisa na asifungiwe kutumia mtandao wa Twitter?", Mtumiaji mmoja aliandika kwa Kiingereza.

"Trump alipigwa marufuku lakini huyu anaachwa tu. Bila shaka huu ni utani sio, au?", Mtumiaji mwingine aliandika.


EmoticonEmoticon