Polisi mjini Moscow wamefanya uvamizi na kuendesha upekuzi mkali kwenye majengo na ofisi zenye mafungamano na familia au washirika wa mwanasiasa wa upinzani aliye kizuizini Alexei Navalny pamoja na kumkamata kaka yake.
Duru kutoka mjini Moscow zimesema maeneo yaliyofanyiwa
upekuzi ni pamoja na makaazi ya Nayalny, ambako kaka yake aitwaye Oleg amekutwa
na kukamatwa, na nyumba nyingine ya kukodi alimokuwa akiishi mke wa mwanasiasa
huyo aitwaye Yulia.
Wakili wa mke
wa Navalny, Veronika Polyakova amewaambia waandishi habari kwamba polisi
haikumruhusu yeye kushiriki uvamizi na upekuzi uliofanyika, jambo ambalo anadai limevunja haki ya mteja wake ya
kuwakilishwa kisheria na kutoa utetezi.
Maeneo
mengine yaliyovamiwa na polisi ni ofisi za wakfu wa Navalny unaoshughulikia
mapambano dhidi ya rushwa na jengo linalotumika kutayarisha video na maudhui ya
mtandaoni ya mwanasiasa huyo wa upinzani.
Polisi pia
ilipekua makaazi ya kiongozi wa muungano wa madaktari nchini Urusi Anastasia
Vasilyeva, ambaye anatajwa kuwa mshirika wa Navalny.
Idara ya polisi haijatoa maelezo yoyote kuhusiana na operesheni yake lakini washirika wa Navalny wamesema kupitia mitandao ya kijamii kwamba wanahusishwa na ukiukaji wa masharti ya afya kwa kuandaa na kushiriki maandamano ya kupinga kuwekwa kizuizini kwa Navalny yaliyofanyika Jumamosi iliyopita mjini Moscow.
EmoticonEmoticon