Raisi Wa Marekani Aruhusu Waliobadilisha Jinsia KuhudumuJeshi

 

Rais Joe Biden ameondoa marufuku iliyowekwa na Donald Trump ya kuwapiga marufuku watu waliobadili jinsia kujiunga na jeshi.

Marufuku hiyo ilitangazwa na Bw. Trump mwaka wake wa kwanza akiwa rais wa Marekani.

''Watumishi waliobadili jinsia hawatakabiliwa na uwezekano wa kuondolewa au kutengwa kwa misingi ya utambulisho wao kijinsia,'' Ilisema ikulu ya White House.

Kulikuwa na askari 8,980 mwaka 2019, kwa mujibu wa takwimu za Idara ya Ulinzi zilizochambuliwa na taasisi ya Palm Center.

''Rais Biden anaamini kuwa jinsia haipaswi kuwa kikwazo kwenye utumishi jeshini, na kuwa nguvu ya Marekani iko kwenye utofauti wa wake,'' Taarifa ya Ikulu iliongeza.

Waziri mpya wa Ulinzi Lloyd Austin, generali wa jeshi mstaafu, alisema kwenye taarifa: ''Idara itatumia sera hii kuhakikisha kuwa watu wanaojipambanua kuwa wamebadili jinsia wanapata uhalali wa kuingia na kutumikia jeshi.''

''Vikosi vya kijeshi vya Marekani vina kazi ya kutetea raia wenzetu dhidi ya maadui, wa nje na ndani. Natumaini tutafanikisha hili vyema ikiwa tutawawakilisha raia wenzetu wote,'' aliongeza.

Bwana Trump alitangaza kupitia ukurasa wa twitter mwaka 2017 kuwa nchi hiyo ''haitakubali au kuruhusu'' kundi hilo la watu kuhudumu kwenye jeshi, akieleza ''gharama kubwa za matibabu na usumbufu''.

Mafufuku hiyo ilianza kufanya kazi mwezi Aprili mwaka 2019. Kundi la watu waliobadili jinsia ambao tayari walikuwa wakilitumikia jeshi waliruhusiwa kuendelea lakini wale waliokuwa wakitaka kujiunga walizuiwa.


EmoticonEmoticon