Raisi Wa Marekani Kusitisha Mauzo Ya Silaha UAE Na Saudi Arabia

 

Utawala wa Rais Joe Biden umesitisha kwa muda uuzaji wa silaha kwa mataifa ya Ghuba. 

Hatua hii inazuia mabilioni ya dola kwa mauzo ya silaha na kubadili maamuzi ya mwisho ya rais aliyeondoka madarakani Donald Trump. Wizara ya mambo ya nje imesema itaikagua mikataba iliyotiwa saini na Trump kabla ya kuibatilisha au kuendelea nayo.

Utawala wa Biden Jumatano umetangaza kuwa utazuilia kwa muda mabilioni ya dola katika mauzo ya silaha kwa Umoja wa Falme za Kiarabu na Saudi Arabia. 

Waziri wa mambo ya Nje, Antony Blinken ameitaja hatua hiyo "kama ya kawaida kiutawala" akibainisha kuwa ilikuwa kawaida kwa utawala unaoingia madarakani kuipitia mikataba mikubwa ya silaha iliyoanzishwa na utawala uliomaliza muda wake.

Wizara hiyo imesema kusitisha kwa muda kutaruhusu utawala wa Biden kuhakikisha mauzo ya silaha za Marekani yanatimiza malengo ya kimkakati ya kujenga washirika wenye usalama, ushirikiano na uwezo.

Blinken katika siku yake ya kwanza ofisini Jumatano, amesema utawala mpya umeanzisha uchunguzi kamili wa uhusiano kati ya Marekani na Urusi pia inachunguza maelezo ya mkataba wa amani wa Marekani na Taliban uliosainiwa karibu mwaka mmoja uliopita.


EmoticonEmoticon