Rais wa
Uganda Yoweri Museveni amethibitisha kuagiza mitandao kadhaa ya kijamii nchini
humo kufungiwa.
Katika hotuba yake iliyooneshwa
mubashara katika televisheni usiku wa Jumanne saa tatu kabla ya muda wa mwisho
wa kufanya kampeni, Rais Museveni aliyekuwa amevalia koti la kijeshi alisema
ameagiza kufungwa kwa mtandao wa kijamii wa Facebook kwa kuwa na kiburi na
kupendelea upande mmoja.
Alisema ikiwa Facebook itatumiwa
nchini Uganda, lazima itumiwe kwa usawa na kila mtu anayetaka kufanya hivyo.
Bw. Museveni pia alisema hatakubali mtu yeyote kucheza na nchi yake ama kuamua
ni nani mzuri au mbaya.
Hatua ya Rais inakuja siku moja baada
ya Facebook kuthibitisha kwamba imezifungia akaunti zinazohusishwa na serikali
iliyo madarakani ikidai kuwa mtandao wake unatumiwa kushawishi mijadala ya umma
katika kinyang'anyiro kikali cha uchaguzi, ambapo rais aliye madarakani na
mpinzani wake mkuu, Robert Kyagulanyi maarufu Bobi Wine wanatafuta ushindi wa
kura za vijana.
Watumiaji wa mitandao ya kijamii ya
Facebook na WhatsApp, Instagram na Snapchat walianza kulalamikia kukatizwa kwa
huduma hizo mapema siku ya Jumanne.
Twitter imejibu hatua hiyo ikisema
kuzingiwa kwa huduma za intaneti ni hatari na inakiuka haki za kimsingi za
binadamu na kanuni ya uhuru wa mawasiliano.
Wakati huo huo Marekani imelaani uamuzi wa serikali kufunga mitandao ya kijamii, huku Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akitoa wito wa kuheshimiwa haki za binadamu.
EmoticonEmoticon