Rais Yoweri
Museveni wa Uganda ameonya watu wenye lengo la 'kumpatanisha' yeye na upande wa
upinzani wa Bobi Wine baada ya kumalizika uchaguzi mkuu uliompa ushindi kuongoza muhula wa
sita.
Huku upande wa upinzani unaoongozwa
na msanii Robert Kyagulanyi maarufu Bobi Wine aliyeshika nafasi ya pili
miongoni mwa wagombea 11 akipinga vikali kutambua matokeo hayo.
Kauli hiyo imekuja baada ya kuibuka
wasiwasi kwa taifa na baadhi ya viongozi wa dini kuomba maridhiano kwa serikali
na upinzani.
Katika maadhimisho ya miaka 35 ya
chama cha NRM kuingia madarakani yaliyofanyika Ikulu ya nchi hiyo siku ya
Jumanne, viongozi wa Kanisa Katoliki katika sala ya kuliombea taifa, waliomba
Rais Museveni kufanya maridhiano na kumuachia kiongozi wa chama cha upinzani
cha NUP, Robert Kyagulanyi aliyekuwa amezuiliwa nyumbani kwake.
Rais Museveni aliwajibu akisema,
serikali ya NRM tayari ilianza maridhiano miaka mingi iliyopita ndio sababu
katika serikali yake kuna mwana wa aliyekuwa Rais wa Uganda, Idi Amin , mwanae
Rais wa zamani Tito Lutwa Okello na wengine wengi.
''Fikiria kuna baadhi ya watu
wanaokuja kwangu wanataka kuwa wapatanishi wangu na upande wa upinzani,
'kunipatanisha' nini? sitaki 'upatanishi' wowote.''Alisema Rais Museveni.
''Kila mtu anafahamu mahala pangu na
mimi ninafahamu mahali upinzani wanapopatikana ninaweza kwenda kwao
tukazungumza, sitaki upatanisho wowote, ni matusi kuniambia unataka
kunipatanisha.'' Aliongeza Museveni .
Kiongozi wa chama cha NUP Robert
Kyagulanyi alipokutana na wabunge wake wateule siku ya Jumanne kwa mara ya
kwanza, aliwataka wapinge matokeo ya uchaguzi mkuu.
''Tuna ushahidi wa kutosha na nyinyi
mnafahamu kuwa Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi alitangaza matokeo ambayo si ya
kweli na kwanza tunapinga udanganyifu huo, na sasa tuko kwenye mazungumzo tuone
kama tunaweza kupeleka kesi Mahakamani''. Alisema Kyagulanyi.
Awali vyombo vya habari nchini humo vilimnukuu Rais Museveni akisema kuwa yuko tayari kufanya maridhiano na yeyote ambaye anamsimamo tofauti na ule wa chama tawala cha NRM.
Credit:Bbc
EmoticonEmoticon