Trump Asema Hatahudhuria Kuapishwa Kwa Biden

 

Rais wa Marekani Donald Trump anayeondoka madarakani, amesema hatahudhuria sherehe za kuapishwa kwa rais mpya Joe Biden hapo tarehe 20 ya mwezi huu. 

Trump amesema hayo wakati ambapo taarifa za vyombo vya habari nchini Marekani zimeashiria uwezekano wa rais huyo kukabiliwa na mashtaka kwa mara ya pili juu ya kumwondoa madarakani baada ya wafuasi wake kulivamia bunge na kufanya fujo.  

Uamuzi wa Trump unakingamana na kauli aliyotoa hapo awali juu ya kuhakikisha mchakato wa kukabidhi madaraka kwa amani. Hata hivyo rais mteule Joe Biden amesema uamuzi huo wa Trump ni jambo zuri kwake.

Shirika la habari la Reuters limekinukuu chanzo katika utawala wa Trump kilichotoa taarifa kwamba huenda rais huyo anayemaliza muda wake ataondoka kutoka kwenye Ikulu siku moja kabla ya sherehe za kuapishwa rais mpya wa Marekani na atelekea katika nyumba yake ya mapumziko jijini Florida.

Wabunge wanatarajiwa kujadili hatua za kuwasilisha nakala za mashtaka kwa Baraza la Wawakilishi kwa ajili ya kupiga kura juu ya madai dhidi ya rais Trump ya kuwachochea waandamanaji waliolivamia jengo la bunge la Marekani. 

Msemaji wa Ikulu, Judd Deere alijibu haraka kwamba kumfungulia mashtaka rais Trump wakati ambapo zimebakia siku 11 tu kabla ya kumalizika kipindi chake cha urais ni hatua itakayoitumbukiza zaidi nchi hiyo katika migawanyiko.


EmoticonEmoticon