Trump Ni Rais Wa Kwanza Marekani Kupigiwa Kura Ya Kushitakiwa Mara Mbili

 

Rais Donald Trump amekuwa rais wa kwanza katika historia ya Marekani kupigiwa kura mara mbili ya kuondolewa madarakani. 

Baraza la wawakilishi liliamua jana kumshitaki Trump, kwa kuchochea uasi katika uvamizi uliofanywa na wafuasi wake katika majengo ya bunge wiki iliyopita. 

Warepublican 10 waliungana na wawakilishi wa Democrats na kusema kwamba kiongozi huyo anatakiwa kuwajibika kwa uvamizi huo. Spika wa baraza la wawakilishi Nancy Pelosi amesema rais Trump ni lazima aondoke kwa kuwa ndiye aliyechochea uasi na ni kitisho kwa nchi. 

Kifungu hicho cha mashitaka sasa kitawasilishwa katika bunge la seneti ambalo bado linadhibitiwa na chama cha Republican na linatarajiwa kukutana tena Januari 19 siku moja kabla, rais mteule Joe Biden aapishwe. 

Zikiwa zimesalia siku chache kabla ya muda wa Trump kumalizika, Wademocrat waliharakisha mchakato wa kutaka kumvua Trump madaraka baada ya makamu wa rais Mike Pence kukataa kuitikia miito ya kutumia ibara ya 25 ya katiba ya nchi hiyo kumuondoa ofisini.


EmoticonEmoticon