Ujerumani Yarefusha Hatua Kali Za Kupambana Na Maambukizi Ya Corona

 

Ujerumani imerefusha muda wa hatua kali za kupambana na kusambaa kwa virusi vya corona hadi tarehe 31 Januari. Uamuzi huo umefikiwa baada ya mkutano kati ya Kansela Angela Merkel na viongozi wa majimbo ya shirikisho. 

Akitangaza hatua hizo Jumanne usiku Kansela Angela Merkel amesema vikwazo vikali zaidi vitawekwa kuzuia watu kutangamana ili kudhibiti ongezeko la maambukizi.

Masharti yatakayotekelezwa nchini kote Ujerumani ni pamoja na kuendelea kuzifunga shule, hali kadhalika biashara na huduma zote zisizo za lazima hadi mwishoni mwa mwezi huu wa Januari. 

Masharti hayo ambayo yaliwekwa katikati mwa mwezi uliopita wa Desemba yalitarajiwa kumalizika tarehe 10 Januari.

Kansela Merkel amesema aina mpya ya virusi vilivyotoka nchini Uingereza, na msimu wa baridi vinaleta changamoto inayohitaji hatua kali za kukabiliana navyo.

''Nimesema mara kwa mara kwamba miezi ya msimu wa baridi, kama walivyotueleza wataalamu jana, ni wakati ambapo athari za janga hili zinaongezeka,'' amesema Kansela Merkel, na kuongeza kuwa kuwepo ''kirusi kilichojibadilisha ambacho tayari kimeonekana nchini humu, inatulazimu kuchukua hatua kali za tahadhari.''


EmoticonEmoticon