Uongozi Wa Biden Waanza Kuchukua Hatua Kupunguza Uchafuzi Wa Hewa

 

Rais Joe Biden amesaini amri kadhaa za utendaji ili kupunguza uchafuzi wa hewa kutokana na mafuta, gesi na mkaa, katika juhudi zake za kukabliana na mabadiliko ya hali ya hewa.

Biden anasema anataka Marekani kwa mara nyingine tena kuongoza dunia katika ajenda ya hali ya hewa, ikiwa ni mabadiliko makubwa kutoka sera za aliyemtangulia.

Mwaka 2020 ulikuwa ni wa joto zaidi kuliko mwaka mwengine ule katika historia ya dunia, kutokana na hali ya kuongezeka kwa joto duniani kufuatana na takwimu za Idara ya Safari za Anga ya Marekani, NASA.

Akiwa na lengo la kupunguza uchafuzi wa hewa unaotokana na mafuta, gesi na mkaa, ili kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa Rais Biden amesema Marekani haiwezi tena kusubiri ili kukabiliana na janga la hali ya hewa duniani akiitaja kuwa ni tishio kubwa kabisa.

Rais Joe Biden aeleza : "Na sawa na jinsi tunavyo hitaji jibu la pamoja la kitaifa kukabiliana na Covid 19, tunahitaji kwa fharura jibu la pamoja la kitaifa kwa ajili ya mzozo wa hali ya hewa, kwa sababu kuna mzozo wa hali ya hewa. Ni lazima tuongoze dunia katika kukabiliana na janga hili."

Hapo jana jioni Rais Biden alisaini amri ya utendaji juu ya masuala ya hali ya hewa, ikiwa ni pamoja na kusitisha kutolewa vibali vipya vya uchimbaji mafuta na gesi na kumaliza ruzuku kwa ajili ya mafuta ghafi. Amri hiyo inachukuwa hatua ya kuhifadhi asilimia 30 ya ardhi ya nchi hii na maji kufikia 2030, na kuelekea katika kutumia magari ya serikali yenye nishati za umeme.


EmoticonEmoticon