Waasi Wauvamia Mji Wa Bangassou Kabla Ya Matokeo Kutangazwa

 

Waasi katika Jamhuri ya Afrika ya Kati wameushambulia mji wa Bangassou, siku moja kabla ya kutangazwa matokeo ya uchaguzi wa rais ulioandamwa na ukosoaji. 

Wanajeshi wa Umoja wa Mataifa wamelisaidia jeshi la serikali ya nchi hiyo dhidi ya waasi hao waliotaka kuudhibiti mji huo wa kusini mashariki jana Jumapili. Ujumbe wa Umoja wa Mataifa katika nchi hiyo, MINUSMA umesema katika taarifa yake, kuwa wapiganaji watiifu kwa rais wa zamani Francois Bozize walihusika katika ghasia hizo za jana. 

Katika ujumbe huo kupitia mtandao wa twitter, MINUSMA imesema wanajeshi wake wameulinda mji wa Bangassou, na kwamba imepatikana miili ya wanamgambo watano waliouawa. 

Mkuu wa ujumbe huo wa kulinda amani, Rosevel Pierre Louis ameliambia shirika la habari la AFP kwamba mji huo wenye machimbo ya almasi ulishambuliwa alfajiri ya jana na kwamba waasi walikuwa wametapakaa kila mahali, huku wanajeshi wa serikali wakiwa wamevikimbia vituo vyao.


EmoticonEmoticon