Bunge la
uwakilishi nchini Marekani limepiga kura ya kutokuwa na imani dhidi ya rais
Donald Trump kwa kuchochea ghasia zilizosababisha uvamizi wa jumba la bunge la
Capitol.
Wabunge 10 wa chama cha Republican walishirikiana na wenzao
wa chama cha Democrat kupitisha kura hiyo ya kumshtaki rais kwa 232 dhidi ya
wabunge 197 waliopinga hatua hiyo.
Ni rais wa kwanza katika historia ya Marekani kupigiwa kura
ya kutokuwa na imani mara mbili ama kushtakiwa kwa makosa ya uhalifu na bunge
hilo la Congress.
Rais Trump ambaye ni mwanachama wa Republican sasa
atakabiliwa na kesi katika bunge la seneti ambapo iwapo atapatikana na hatia
huenda akapigwa marufuku kushikilia wadhfa wowote wa ofisi ya umma.
Bwana Trump
anaachia madaraka tarehe 20 mwezi Januari kufuatia kushindwa kwake katika
uchaguzi mkuu mwezi Novemba uliomtangaza Joe Biden mshindi.
Bunge hilo linalodhibitiwa na wabunge wengi wa Democrat
lilipiga kura siku ya Jumatano saa kadhaa baada ya mjadala mkali huku walinzi
wa kitaifa wakiimarisha usalama ndani na nje ya jumba la bunge hilo.
Shirika la kijasusi nchini Marekani FBI limeonya kwamba kuna
uwezekano wa kuzuka kwa maandamano katika majimbo yote 50 kabla ya kuapishwa
kwa rais mteule Joe Biden wiki ijayo.
Katika kanda
ya video iliotolewa baada ya kura hiyo kupigwa , bwana Trump aliwataka wafuasi
wake kusalia watulivu lakini hakuzungumzia kwamba alikuwa amepigiwa kura ya
kutokuwa na imani naye bungeni.
'Ghasia na uharibifu hauna nafasi katika taifa letu…hakuna mfuasi wangu ambaye angependelea kufanyika kwa ghasia za kisiasa' , alisema akionesha huzuni na mwenye kutaka maridhiano.
EmoticonEmoticon