Wanajeshi Waondoka Nyumbani Kwa Bobi Wine

 

Majeshi ya Uganda yameondoka kwenye makaazi ya kiongozi wa upinzani Robert Kyagulanyi, maarufu Bobi Wine na kumaliza kuizingira nyumba yake tangu alipowekwa katika kizuizi cha nyumbani Januari 14.

Majeshi hayo yameondoka baada ya mahakama jana kuwaamuru polisi na wanajeshi kuondoka kwenye nyumba ya Bobi Wine iliyoko mjini Kampala.

Mwandishi habari wa Reuters aliyekuwepo eneo la tukio, amethibitisha kwamba majeshi hayo yameondoka, ingawa mwanasiasa huyo wa upinzani hakuwa bado ameonekana kwenye maeneo hayo.

Bobi Wine, mwenye umri wa miaka 38 alikuwa katika kizuizi cha nyumbani tangu siku ya uchaguzi mkuu wa Januari 14, baada ya vikosi vya usalama kudai kuwa vilikwenda kwenye makaazi yake kwa ajili ya kumlinda.

Uchaguzi huo mkuu wa Uganda, ulimpa ushindi Rais Yoweri Museveni, matokeo ambayo yamepingwa na Bobi Wine, akidai kuwa uligubikwa na udanganyifu.


EmoticonEmoticon