Al-Shabab Wavamia Hoteli Mogadishu, Somalia

 

Wanamgambo wa Al-Shabab nchini Somalia wamehusika katika makabiliano ya polisi na vikosi vya usalama katika hoteli moja iliyopo mji mkuu wa Mogadishu.

Kundi la Al-Shabab limekiri kutekeleza shambulizi hilo katika hoteli ya Afrik ambalo lilianza na bomu lililokuwa limetegwa kweye gari Jumapili mchana.

Hadi kufikia sasa, haijafahamika ni watu wangapi waliojeruhiwa lakini shirika la habari la AFP limeripoti kuwa karibu watu watatu wamefariki dunia.

Kundi hilo ambalo linahusishwa na kundi la wanamgambo la Al-Qaeda, mara nyingi hutekeleza mashambulizi dhidi ya serikali.

Inasemekana kuwa gari moja liligonga eneo la mbele la hoteli hiyo na kulipuka kabla ya mshambuliaji aliyekuwa amejihami kwa silaha kuvamia jengo la hoteli, kulingana na maafisa na wengine walioshuhudia shambulizi hilo.

"Mlipuko huo ulifanya hoteli hiyo ikaanza kutetemeka wakati tukiwa ndani tunaendelea na mzungumzo. tulishutuka, tusijue la kufanya," aliyeshuhudia Ahmed Nur amenukuliwa na shirika la habari la Reuters.

Maafisa waandamizi wa usalama Mohamed Dahir ameliambia shirika la AFP kuwa raia wawili na afisa mmoja wa usalama wamethibitishwa kufariki dunia, "lakini idadi ya waliofariki huenda ikaongezeka."


EmoticonEmoticon