Baraza La Usalama Litakutana Kujadili Mapinduzi Ya Myanmar

 

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linapanga kukutana Jumanne kujadili mapinduzi ya Myanmar. Aidha umoja huo unahofia mapinduzi yanaweza kuhatarisha zaidi maisha ya Warohingya Waislamu katika jimbo la Rakhine. 

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa litafanya mkutano wa dharura kujadili mapinduzi ya kijeshi yaliyotokea nchini Myanamar.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameyaeleza mapinduzi hayo kuwa ni pigo kubwa kwa demokrasia ya Myanmar.

Mkutano huo utakaofanyika Jumanne unatarajiwa kujadili hatua za kuulinda uchaguzi wa Novemba 8 uliokipa ushindi chama tawala, pamoja na kuhakikisha kiongozi wake Aung San Suu Kyi anaachiliwa huru na wenzake kadhaa waliokamatwa na jeshi. 

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephen Dujarric amesema umoja huo umeshindwa kuwasiliana na maafisa wa kijeshi wa Myanmar wala viongozi waliowakamata.

Dujarric ameongeza kwamba mapinduzi hayo yanaweza kuifanya hali kuwa mbaya zaidi kwa Warohingya 600,000 waliobakia katika jimbo la Rakhine.

"Kuna takriban Warohingia 600,000 waliobakia katika jimbo la Rakhine, pamoja na watu 127,000 walio kwenye kambi. 

Hawawezi kuondoka na hawana hata huduma za msingi za afya na elimu. Kwa hivyo hofu yetu ni kwamba tukio hili linaweza kufanya hali kuwa mbaya zaidi kwao," amesema Dujarric.

Kufuatia kampeni ya kijeshi ya mwaka 2017, Waislam wa kabila ya Rohingya wapatao 700,000 walilikimbia jimbo hilo la Rakhine na kwenda Bangladesh, ambako bado wamekwamba kwenye kambi za wakimbizi.


EmoticonEmoticon