Barcelona Yasikitishwa Na Kuvuja Kwa Mkataba Wa Messi, Waahidi Kufungua Kesi

 

Barcelona imesema kuwa itachukua "hatua za kisheria" dhidi ya gazeti la Uhispania la El Mundo baada ya kuchapisha maelezo kuhusu mkataba wa mshambuliaji, Lionel Messi wa pauni milioni 492.

Barcelona ilikanusha kuhusika kwa namna yoyote ile katika uchapishaji wa taarifa hizo.

Kwa mujibu wa El Mundo, mkataba wa Messi wa miaka minne ulikuwa wa thamani ya takriban euro 555,237,619 hadi Juni 30, 2021.

Hii inamaanisha kuwa kijana huyo mwenye umri wa miaka 33, atakuwa anapokea pauni milioni 123 kwa msimu.

Barcelona imesema katika taarifa iliyotoa kuwa "inasikitishwa na uchapishaji wa maelezo hayo". Na kuongeza kuwa: "FC Barcelona haihusiki kwa namna yoyote ile katika uchapishaji wa taarifa hiyo na itachukua hatua stahiki za kisheria dhidi ya gazeti la El Mundo, kwa uharibifu wowote ule ambao huenda umetokea kwasababu ya taarifa hiyo.

"FC Barcelona imeonesha kumuunga mkono Lionel Messi, hasa katika jaribio lolote la kumdhalilisha na kuharibu uhusiano wake katika klabu hiyo ambako amefanyakazi na kuwa mchezaji bora duniani na katika historia ya soka."

Mchezaji huyo wa kimataifa wa Argentina Messi alijiunga na Barcelona akiwa na umri wa miaka 13 lakini akatuma ombi la kutaka aruhusiwe kuhamia kwingineko mnamo mwezi Agosti.

Bado haijafahamiki ikiwa atabaki katika klabu hiyo wakati mkataba wake utakapomalizika.


EmoticonEmoticon