Chama Kimoja Japani Chapiga Marufuku Wanawake Kuzungumza Mikutanoni

 

Siku kadhaa baada ya mkuu wa michezo ya Olimpiki nchini Japani kulazimishwa kujiuzulu kwasababu ya maneno yake ya kudhalilisha wanawake, chama chake kimeamua kualika wanawake kuhudhuria mikutano muhimu - mradi tu wasiseme neno.

Chama cha Liberal Democratic (LDP) kilipendekeza wabunge wanawake washuhudie bodi ambayo ina wanaume tu namna wanavyoendesha mkutano wao.

Hawaruhusiwi kuzungumza wakati wa mkutano - lakini wanaweza kutoa maoni yao baadaye.

Wanawake nchini Japani kwa kipindi kirefu wamekuwa wakijitenga na ushiriki wa kisiasa na kiuchumi.

Nchi hiyo imeorodheshwa kuwa ya 121 kati ya nchi 153 kulingana na kipimo cha Jukwaa la Kiuchumi Duniani mwaka 2020 cha tofauti la kijinsia Duniani.

Wanawake wawili sasa hivi ndio wanaoshiriki katika bodi ya watu 12 ya chama cha LDP ambacho kimekuwa madarakani karibu kila wakati tangu mwaka 1955.

Toshihiro Nikai, 82, katibu mkuu wa chama cha LDP, amezungumza na wanahabari Jumanne kwamba anataka kukaribisha wanawake katika mkutano huo.

Alisema anafahamu ukosoaji unaoendelea dhidi ya wanaume kutawala bodi ya chama hicho na ilikuwa muhimu kwa wanachama wa kike wa chama hicho kufuatilia mchakato wa maamuzi unavyoendeshwa, alinukuliwa na shirika la habari la Reuters

"Ni muhimu kuelewa majadiliano yanavyoendelea. Kutazama na kufuatilia," alisema.

Chombo cha habari nchini Japani kimesema wanawake watano huenda wakaruhusiwa kuketi na kufuatilia mkutano wa bodi inayofanya maamuzi lakini hawataruhusiwa kuzungumza. Wanaweza kuwasilisha maoni yao baadaye kwa Sekretarieti.

Sasa hivi wanasiasa 46 kati ya 465 nchini Japani ndio waakilishi wa wanawake - hiyo ikiwa ni takriban asilimia 10 ikilinganishwa na asilimia 25 kote duniani.


EmoticonEmoticon