Rais wa Marekani Joe Biden
ametishia kuirejeshea Myanmar vikwazo baada ya jeshi kupindua serikali.
Jeshi la Myanmar lilimkamata Aung San Suu Kyi na viongozi wengine wa
kisiasa wakiwashutumu kwa udanganyifu katika uchaguzi wa hivi karibuni ambao
Suu Kyi alipata ushindi mkubwa.
Katika taarifa, Bwana Biden amesema "nguvu isiwahi kutumika
kubadilisha maamuzi ya watu au kufuta matokeo ya uchaguzi uliofanyika kwa njia
ya halali".
Umoja wa Mataifa na Uingereza pia zimeshutumu mapinduzi hayo.
Marekani ilikuwa imeiondolea
nchi hiyo vikwazo zaidi ya muongo mmoja uliopita wakati ambapo Myanmar
ilionesha kufuata demokrasia.
Bwana Biden amesema hatua hiyo itapitiwa tena kwa haraka na kuongeza:
"Marekani itaunga mkono demokrasia kila itakapokuwa hatarini."
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres aliitaja hatua
iliyochukuliwa na jeshi "pigo kubwa kwa mabadiliko ya kidemokrasia",
huku baraza la usalama likijitayarisha kufanya mkutano wa dharura.
Umoja wa Mataifa imetaka kuachiliwa kwa watu wasiopungua 45 ambao wanazuiliwa na jeshi.
EmoticonEmoticon