Raisi Wa Marekani Atangaza Muelekeo Mpya Wa Siasa Za Nje Za Marekani

 

Rais Joe Biden wa Marekani ametangaza muelekeo mpya wa sera za nje za nchi yake, akijaribu kujiondowa kwenye njia ya uhasama na kujitenga iliyofuatwa na mtangulizi wake, Donald Trump. 

Akitangaza kile alichokiita kurejea rasmi kwa Marekani kwenye uwanja wa diplomasia ya kilimwengu, Biden aliwaambia wanadiplomasia kwenye Wizara ya Mambo ya Kigeni ya nchi yake kwamba wana jukumu kubwa la kurekebisha mule mote mulimovurugwa panapohusika taswira ya taifa lake duniani:

"Marekani imerehea. Marekani imerejea. Diplomasia imerejea kwenye kiini cha sera yetu ya mambo ya nje. Kama nilivyosema kwenye hotuba yangu ya kuapishwa, tutarekebisha mahusiano na washirika wetu, na tutajihusisha tena na ulimwengu sio kwa kukabiliana na changamoto za jana, bali za leo na za kesho," alisema kiongozi huyo.

Mahsusi kabisa, Biden alitumia hotuba hiyo kuonesha utayari wa serikali yake kuhakikisha kuwa Marekani inasimama imara mbele ya mahasimu wake wa jadi, Urusi na China, lakini kwa njia ambazo hazitahatarisha mataifa mengine. 

Biden alisema Marekani na Urusi zimekubaliana kuongeza muda wa mkataba mpya wa kusitisha mashindano ya silaha kati yao kwa kipindi cha miaka mitano, na hivyo kuulinda mkataba pekee kati ya nchi hizo juu ya nyuklia.

"Nimemwambia wazi Rais Putin kwamba mimi ni tafauti sana na mtangulizi wangu, lakini siku za Marekani kuvivumilia vitendo vya Urusi kuuingilia uchaguzi wetu, mashambulizi ya mitandaoni, kuwapa sumu raia wake, zimekwisha. Hatutasita kuifanya Urusi ilipie gharama za hayo na kuyalinda maslahi na watu wetu," alisisitiza.


EmoticonEmoticon