Viongozi Wa Ulaya Kutoondoa Haraka Vizuizi Vya Covid-19

 

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wamesema kuwa vizuizi vikali vya kusafiri vinapaswa kuendelea kutekelezwa wakati kanda hiyo ikapambana kuuweka sawa mpango wake wa kutoa chanjo ya virusi vya corona unaosuasua. 

Katika taarifa ya pamoja iliyotolewa baada ya mkutano wa kilele wa siku mbili ulioanza jana kwa njia ya video, viongozi 27 wa mataifa wanachama wa Umoja wa Ulaya wamesema hali ya janga la corona bado inatia wasiwasi na aina mpya ya virusi hivyo inaongeza mfadhaiko.

Wamekubaliana kuendelea na vizuizi vilivyopo huku wakizidisha kasi na kuimarisha mpango wa utoaji wa chanjo ambao unakwenda kwa mwendo wa konokono kutokana na uhaba wa chanjo uliopo.

Viongozi wakuu wa Umoja wa Ulaya wamewaambia Waandishi Habari kuwa itachukua miezi kadhaa kabla ya kanda hiyo kufikia uwezo wa kusambaza chanjo za kutosha za virusi vya corona.

Hata hivyo rais wa Halmashauri kuu ya Umoja wa huo Ursula von der Leyen amesema "Tunaamini kuwa tunaweza kufikia lengo letu la kutoa chanjo kwa asilimia 70 ya idadi ya watu wazima ifikapo mwishoni mwa majira ya kiangazi. Hao ni watu milioni 255 ndani ya Umoja wa Ulaya na tukiangalia takwimu zetu, hilo ni lengo tunaloweza kulifikia."


EmoticonEmoticon